JE! CHAKULA KINAWEZA KUATHIRI AKILI YAKO? (SOMA DANIELI 1 YOTE)


Amini usiamini, chakula kinaweza kuathiri akili yako, na
afya yako ya kimwili na kiroho. Kwa maelezo zaidi juu ya somo
hili la afya soma vitabu vya Afya na Lishe, kama vile Afya na
Raha na Uponyaji wa Mungu ambamo zimefafanuliwa Kanuni 8 za
Afya ----- Lishe bora, Mazoezi ya mwili, Hewa safi, Maji safi
na salama, Mwanga wa jua, Pumziko, Kiasi, na Kumwamini Mungu.
Ukizifuata utaepukana na magonjwa mengi na kupunguza gharama ya
matibabu. Yatabaki magonjwa yanayokuja kwa njia zingine
zisizozuilika.
Chakula cha daraja la kwanza ambacho Mungu alimpa mwanadamu
kilikuwa cha nafaka, kokwa na matunda (Mwanzo 1:29). Dhambi
ilipoingia ilileta laana sio tu kwa viumbe vyote bali hata kwa
ardhi. Kwa hiyo Mungu akamwongezea mwanadamu mboga za majani
katika lishe yake ya awali (Mwanzo 3:18). Gharika ilikaa juu ya
nchi kwa miezi mitano au siku 150 na kuharibu mimea yote (Mwanzo
7:24). Kwa hiyo Mungu akamwongezea mwanadamu katika lishe yake
"nyama" kutoka kwa wanyama safi tu (Mwa. 8:3,4 imebainishwa na
Law. 11:1-47; Kum. 14:1-21). Injini ya petroli hutumia petroli
tu; injili ya dizeli ni dizeli tu. Ukitaka gari lako life weka
dizeli katika injini ya petroli au petroli katika injini ya
dizeli. Mtengenezaji ndiye anayejua gari lake litatumia mafuta
gani, sio mtumiaji. Vile vile, Mungu anajua chakula kinachofaa
kwa mwili wa mwanadamu, sio mwanadamu kujichagulia cho chote
kuwa chakula. Wabishi wataharibu injini za magari yao (miili
yao).
Mungu aliumba wanyama safi na wanyama najisi juma lile la
kwanza la uumbaji. Kifo cha Yesu msalabani hakikuwa kwa kusudi
la kuwabadilisha wanyama najisi kuwa wanyama safi, bali wanadamu
wenye dhambi kuwa watakatifu. Wale wanaotaka kuwa watakatifu
watajiepusha kula nyama inayotokana na wanyama najisi; lakini
wale wasiotaka utakatifu wataswaga kila kitu (Law.
11:41,43,46,47; Kum. 14:1-4). Mungu hamlazimishi mtu, kama
vile mtengenezaji wa injini ya gari asivyomlazimisha mtu kutumia
mafuta aliyopendekeza. Lakini matokeo mwilini ni ya hakika.
Kisa cha Petro katika Matendo 10:9-16 kimetafsiriwa chini
yake katika fungu la 25 hadi 29. Hayo yalikuwa ni maono tu, si
kitu halisi; hata hivyo Petro alikataa katakata kuchinja na
kula wanyama najisi ingawa ni Mungu mwenyewe aliyemwamuru
kufanya hivyo mara tatu. Mungu hana kigeugeu; alisema wanyama
najisi wasiliwe, basi, hawawezi kuliwa milele (Mal. 3:6; Zab.
89:34). Watu wanamsingizia bure Petro wanapochinja wanyama
najisi na kula; yeye alikataa katakata. Lakini kuna adhabu
kali sana kwa wale wanaoendelea kula nguruwe, panya, na
machukizo yote ya Mataifa (wapagani). Soma Isaya 65:2-6;
66:15-17).
Pombe haikuwa sehemu ya kinywaji ambacho Mungu alimpa
mwanadamu; maji safi na salama ndicho kinywaji bora kuliko
vyote kwa mwanadamu (Mithali 20:1; 23:29-35). Walevi
hawataurithi ufalme wa Mungu (1 Kor. 6:9,10; Gal. 5:21). Kuna
wengi wanaosema, "Mimi nakunywa sana, lakini silewi." Tatizo
la pombe sio kulewa tu, bali ni zile athari zinazotokana na
kunywa pombe ambayo ina sumu mbaya ya alkoholi. Sumu hiyo
huathiri vibaya moyo, mishipa ya fahamu, nyama za mwili na
kadhalika. Mungu atamharibu mtu ye yote anayeuharibu mwili wake
kwa makusudi kwa njia yo yote ile ----- pombe, tumbako, madawa
ya kulevya, na kadhalika (1 Kor. 3:16,17). Pia kuna vinywaji
vinavyopendwa na watu wengi aina ya 'Cola', Kahawa, na Majani ya
Chai ambavyo huidhuru mishipa ya fahamu, ubongo na mwili.
Viepukwe.
Hebu sasa na tuwaangalie wale vijana wanne wa Kiebrania,
mateka kutoka Yerusalemu, wakiwa katika jiji lile la Babeli
mwaka ule wa 606 au 605 K.K. Walikuwa na umri kati ya miaka 18
na 20. Kutokana na hekima yao walichaguliwa kujiunga na vijana
wengine wa Babeli katika Chuo cha Kishenzi [Kipagani] cha Babeli
kwa mafunzo ya miaka mitatu. Wakapewa majina ya miungu ya
Babeli ----- Danieli akaitwa Belteshaza, Hanania akaitwa
Shadraka, Mishaeli akaitwa Meshaki, na Azaria akaitwa Abednego
(Dan. 1:6,7). Mfalme akaamuru wale chakula cha mfalme ili
wanenepe na kuwa na akili nyingi. Kusudi lake lilikuwa zuri
sana. Lakini, je! chakula kile cha mfalme ambacho kilikuwa na
nyama najisi, kilikolezwa kwa viungo vingi vinavyodhuru mwili,
na huenda kilikuwa na vileo kingeweza kuleta afya bora na akili
safi? (Dan. 1:1-5). Vijana hao wanne wa Kiebrania walikuwa
wamelelewa katika mazingira tofauti. Walifuata kanuni za afya
na chakula ambacho Mungu aliwapa wanadamu kula. Walijiepusha na
nyama ya aina yo yote ile pamoja na divai (maji matamu ya
zabibu) kwa vile wao walikuwa wanadhiri wa Bwana (Hesabu 6:1-5).
Kwa hiyo agizo hilo la mfalme kwao likawa mtihani mgumu sana.
"Danieli aliazimu moyoni mwake ya kuwa hatajitia unajisi
kwa chakula cha mfalme, wala kwa divai aliyokunywa; basi
akamwomba yule mkuu wa matowashi ampe ruhusa asijitie unajisi"
(Dan. 1:8). Ni ujasiri ulioje! Ombi lake halikuwa rahisi
kukubaliwa na msimamizi yule kwa vile angekatwa kichwa kama
wangeonekana wamekondeana (Dan. 1:10). Basi Danieli akamwambia,
"Tafadhali utujaribu sisi watumishi wako muda wa siku kumi; na
watupe mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda] tule, na
maji tunywe. Kisha nyuso zetu zitazamwe mbele yako, na nyuso za
wale vijana wanaokula chakula cha mfalme..." (Dan. 1:13).
Akawakubalia ombi hilo. Je! mambo yalikuwaje kiafya baada ya
siku zile kumi tu? "Nyuso zao zilikuwa nzuri zaidi [wanawake
wanaohangaika na vipodozi vinavyodhuru afya wangezingatia hilo],
na miili yao ilikuwa imenenepa zaidi, kuliko wale vijana wote
waliokula chakula cha mfalme. Basi yule msimamizi akaiondoa
posho yao ya chakula [cha mfalme], na ile divai waliyopewa
wanywe, akawapa mtama [nafaka, kokwa, mboga za majani, matunda]
tu" (Dan. 1:15,16).
Chakula cha matajiri au wafalme tunachokitamani sana
hakileti afya mwilini. Chakula rahisi cha mimea na maji safi na
salama ni lishe bora. Kwa akili safi na mwili wenye afya,
ulionenepa kiafya sio kwa ugonjwa, tumia vyakula vya mimea na
maji safi na salama, na kufuata Kanuni zile 8 za Afya. Wana
sayansi wamegundua kuwa wale wanaokula vyakula vya mimea bila
nyama wanaishi maisha marefu sana kuliko wanaokula nyama.
Danieli naye aliishi zaidi ya miaka 80 kufikia kipindi cha
utawala wa Koreshi (Dan. 1:21; 10:1). Hebu tuwafuatilie vijana
wale wanne mwisho wa mafunzo yao ya miaka mitatu. Mfalme
Nebukadreza aliwaonaje?
"Naye mfalme akazungumza nao; na miongoni mwao wote
hawakuonekana waliokuwa kama Danieli, na Hanania, na Mishaeli,
na Azaria... Na katika kila jambo la hekima na ufahamu
alilowauliza mfalme, akawaona kuwa wanafaa mara kumi zaidi ya
waganga na wachawi waliokuwa katika ufalme wake" (Dan.1:19,20).
Kwa nini tuhangaike sana na suala la afya ya mwili wetu,
je! maisha ya kiroho si bora zaidi? "Mpenzi naomba ufanikiwe
katika mambo yote na kuwa na afya yako [kimwili], kama vile roho
yako ifanikiwavyo" (3 Yohana 2). Wahenga walisema, "Akili
timamu katika mwili wenye afya." Ni shauri la kuzingatiwa sana.
Kanuni ya Biblia ni hii: "Basi, mlapo, mnywapo, au mtendapo
neno lo lote fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu" (1 Kor. 10:31).
Tunawajibika kuitunza miili yetu katika hali ya afya nzuri
kadiri iwezekanavyo (l Kor. 6:19,20; 1 Pet. 1:18,19;
Rum.12:1,2). Suala la afya linahusu wokovu wetu. Mungu anaweza
kututumia kama Danieli (Dan. 1:17).

Comments

Popular posts from this blog

SAIKOLOJIA : PATA KUFAHAMU MAKUNDI MANNE YA TABIA ZA BINADAMU.

Rapa B.o.B ataka kuthibitisha iwapo dunia ni duara

Kanuni za kuishi na Watu / Binadam Vizuri