MFALME WA AMANI ANAKUJA UPESI SANA (SOMA DANIELI 2 YOTE)


Hakuna mwanadamu ye yote awezaye kutabiri kwa hakika mambo
yatakayokuja baadaye kwa hekima au maarifa yake mwenyewe.
Wanajimu [wanaobashiri kwa kuangalia nyota], wachawi wanaotazama
bao, wasoma viganja, hata wana sayansi wanabahatisha tu,
hawawezi kujua kwa hakika mambo ya zamani au mambo yanayokuja
mbele (Dan.2:27,28; Isa. 42:8,9; 46:9,10; 41:21-24; 8:19; Yak.
4:13-16).
 Ni Mungu peke yake anayejua mambo ya zamani na yale
yajayo, naye anatuambia kabla hayajatokea. Tangu dhambi iingie
duniani mawasiliano ya moja kwa moja na Mungu yalikatika;
anawasiliana nasi kupitia kwa manabii anaowachagua mwenyewe
(Isa.59:2; Hes. 12:6). Matukio yote makubwa yanayoleta maafa
kwa wanadamu anawajulisha manabii wake (Amosi 3:7). Kuhusu
Gharika alimjulisha Nuhu; kuangamizwa kwa Ninawi alimjulisha
Yona; kuangamizwa kwa Sodoma na Gomora alimjulisha Ibrahimu.
Mbele yetu kuna mapigo saba (Ufunuo 16) ambayo yatawaathiri sana
wanadamu. Kabla hayajaja alimjulisha Yohana kisiwani Patmo.
Maafa yaliyotiishiwa yanaweza kuepukwa kama watu wanaohusika
watatubu na kuacha dhambi zao (Yer. 18:7-10; Yona 3:1-10).
Tukiwakataa manabii wanaotumwa na Mungu hatutafanikiwa
katika safari yetu ya mbinguni (2 Nya. 20:20). Japo vitabu vya
Biblia vilifungwa (Vitabu 66 - Agano la Kale 39; Agano Jipya
27), bado manabii wataendelea kutumwa na Mungu kulionya kanisa
lake (Yoeli 2:28-31; Efe.4:11-14). Kwa kuwa wako manabii wa
uongo, basi, yatupasa kuwapima. Viko vipimo vinne ambayo nabii
ni lazima atimize vyote kuweza kukubalika kama nabii wa kweli wa
Mungu ----- 1. Yer. 28:9; Kum. 13:1-5; 2. Isa. 8:20
[Kut.20:3-17]; 3. Mt. 7:20; 4. 1 Yoh. 4:1-3).
 Unabii na Historia vinakwenda bega kwa bega (Yohana 14:29). Tafsiri
sahihi ya unabii itaungwa mkono na mafungu ya Biblia na Historia
(Isa. 28:10; 2 Pet. 1:19-21). Unabii hautafsiriwi kama mtu
apendavyo au kama kanisa fulani lipendavyo.
Ndoto aliyoota mfalme iliyomfadhaisha sana ilihusu Falme
Kuu Nne zilizotawala dunia na Falme zilizofuata hadi kuja kwa
Yesu Kristo kuja kusimamisha ufalme wake wa milele. Tafsiri ni
hii:-

I. UFALME WA BABELI (606-538 au 605-539
K.K.).
Umewakilishwa na Kichwa cha dhahabu (Dan. 2:37-38).
Historia inaunga mkono.

II. UFALME WA WAMEDI NA WAAJEMI (538-331
au 539-331 K.K.).
Uliuangusha Ufalme wa Babeli (Dan. 5:25-31). Unawakilishwa
na Kifua na Mikono ya Fedha (Dan. 2:32a,39a). Historia inaunga
mkono. Miaka ni ya kukadiria tu.

III. UFALME WA WAYUNANI (331-168 K.K.)
Ufalme wa Wamedi na Waajemi ulitabiriwa kuwa utaangushwa na
Wayunani (Dan. 8:4-7,20-21; 11:1-3). Ufalme wa Wayunani
(Wagiriki) unawakilishwa na Tumbo na Viuno vya Shaba (Dan.
2:32b,39b). Historia inaunga mkono.

IV. UFALME WA WARUMI (168 K.K. - 476 B.K.).
Ufalme wa Warumi unawakilishwa na Miguu ya Chuma. Biblia
inaielezea vizuri Dola ya Warumi kuwa ilikuwa inazivunja-vunja
falme zile nyingine kama chuma. Danieli hakujulishwa jina la
Dola hii. Lakini historia inathibitisha kuwa Warumi
waliwashinda Wayunani mwaka ule wa 168 K.K. Wakati Kristo
anazaliwa Dola hiyo ilikuwa bado inatawala dunia pamoja na
Palestina chini ya Kaisari Augusto (Luka 2:1-7; Yohana 11:48).

V. UFALME WA PAPA (538-1798 B.K.)
Ulitokea katika mabaki ya Dola ya Warumi baada ya
kuangushwa na makabila ya kishenzi [kipagani] ya Ulaya Kaskazini
mwaka wa 476 B.K. Unawakilishwa na Nyayo za miguu
(Dan.2:33b,41a). Udongo unawakilisha kanisa au watu wa Mungu
(Isa.64:8; Yer. 18:6). Chuma kinawakilisha serikali. Hivyo
kuchanganyika kwa udongo na chuma ni muungano wa dini na
serikali chini ya kiongozi mmoja wa kidini wa Roma. Historia
inathibitisha kwamba ufalme huu uliinuka katika mabaki ya Dola
ya Warumi baada ya kuangushwa na kutawala dunia kuanzia 538 B.K.
Huu ni Utawala wa Papa au Upapa.

VI. FALME KUMI ZA ULAYA MAGHARIBI
(476-MAREJEO YA KRISTO)
Falme kumi za Ulaya Magharibi zinawakilishwa na Vidole Kumi
Vya Nyayo (Dan. 2:42). Falme hizo ni Uingereza, Ufaransa,
Ujerumani, Uswisi (Switzerland), Ureno, Hispania, Italia,
Waheruli (Heruli)*, Wavandali (Vandals)*, na Waostrogothi
(Ostrogoths)*. Falme tatu za mwisho huwezi kuziona katika
ramani ya siku hizi. Habari zake zitatolewa katika somo la
Danieli 7. Mataifa hayo 10 yalikuwa makoloni ya Warumi. Rumi
ilipoanguka mwaka 476 yakawa yamejikomboa na kuwa huru. Baadaye
yalipoipokea dini ya Katoliki kwa nguvu yakajikuta yametawaliwa
na Papa aliyejiita Mfalme wa wafalme kuanzia mwaka 538 B.K.

VII. UFALME WA MILELE WA KRISTO (MAREJEO
YAKE HADI MILELE)
Ufalme huo unawakilishwa na Jiwe lililochongwa bila kazi ya
mikono (Dan.2:34,35,44,45). Jiwe hilo ni Kristo (Luka 20:17,18;
Mt. 21:42,44; Mdo. 4:10-12). Huyo ndiye Mfalme wa Amani
anayekuja upesi sana (Isa. 9:6; Ufu.22:12). Atakapokuja
atazivunjilia mbali falme zote za dunia (Ufu.11:15; 19:11-21).
Soma katika kitabu cha Majibu kwa Mashaka Yako somo la miaka
1000 itakayoanza atakapokuja Kristo mara ya pili. Baada ya
kupita miaka hiyo 1000 waovu watafufuliwa na kuangamizwa katika
moto wa milele pamoja na Shetani na malaika zake na kuwa majivu,
ndipo dunia hii iliyoharibiwa vibaya wakati wa kuja kwake mara
ya pili [Yer. 4:23-27; Ufu. 6:14-17] itakapofanywa kuwa mpya
pamoja na mbingu yake (Ufunuo Sura ya 20; Mal. 4:1-3; Eze.
28:14-19; Ufu. 21:1; Zaburi Sura ya 37).
Ombi letu la dhati lingekuwa ni hili: "Ee Yesu, nikumbuke
utakapoingia katika ufalme wako" (Luka 23:42). Ahadi ile ile
itatolewa kwetu kuanzia leo tunapomwomba ombi hilo kama kweli
tumedhamiria kuishi kwa ajili yake hapa duniani, "Utakuwa
pamoja nami peponi" (Luka 23:43). Ndugu yangu, kwa nini leo hii
uipoteze nafasi hii ya thamani? Kata shauri sasa kumfanya Yesu
awe Bwana na Mwokozi wako. Itumie vizuri nafasi ya leo kama
yule jambazi pale msalabani. Acha kucheza na dhambi. Leo ndiyo
siku ya wokovu wako (2 Kor. 6:2).

Comments

Popular posts from this blog

SAIKOLOJIA : PATA KUFAHAMU MAKUNDI MANNE YA TABIA ZA BINADAMU.

Rapa B.o.B ataka kuthibitisha iwapo dunia ni duara

Kanuni za kuishi na Watu / Binadam Vizuri