Magari matatu yatumika kumshusha "LISSU"
MWANASHERIA Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amekamatwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.
Lissu alikuwapo mahakamani hapo asubuhi kwa ajili ya kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili yeye pamoja na wahariri wa gazeti la Mawio ambao ni Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Washitakiwa hao wanaodaiwa kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho ‘Machafuko yaja Zanzibar’. Licha ya kesi hiyo kuahirishwa hadi Alhamisi wiki hii, Lissu alikuwa anamwakilisha mfanyabiashara Yericko Nyerere, anayekabiliwa na mashitaka ya uchochezi iliyopo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Baada ya kutoka mahakamani hapo, Lissu akiwa nje ya mahakama alikuwa akizungumza na mwanasheria mwenzake, Peter Kibatala ambapo baadaye aliingia kwenye gari lake lenye namba za usajili T 216 DHH.
Wakati akitaka kutoka mahakamani hapo, gari la polisi lenye namba RX04 EZN aina ya Land cruiser lilimzuia kupita getini huku gari lingine la Polisi lenye namba za usajili T 475 BNM lilimzuia kwa nyuma likiwa na askari wenye silaha.
Pia nje ya geti la mahakama hiyo, kulikuwa na gari lingine lenye namba za usajili T 424 BZN na kufanya idadi ya magari yaliyomzuia Lissu kuwa matatu ambapo baadaye askari walishuka na kumweka chini ya ulinzi huku wakimtaka ashuke apande gari lao ili kwenda Kituo Kikuu cha Polisi.
Katika mahakama hiyo, Lissu anakabiliwa na kesi zaidi ya tano ambazo zote ni za uchochezi, na mwisho alipandishwa kizimbani Julai 24, mwaka huu. Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya alisema hana taarifa za kukamatwa kwa mbunge huyo.
Wakati huohuo Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya (Chadema) amepokewa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili juzi saa tano usiku akitokea hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara na amelazwa katika wodi namba 18 Sewahaji baada ya kuzidiwa akiwa Kituo Kikuu cha Polisi cha Tarime.
Comments
Post a Comment